JINSI ULAJI WA TENDE UNAVYOSAIDIA LEBA YA UZAZI

JINSI ULAJI WA TENDE UNAVYOSAIDIA LEBA YA UZAZI




✍️Abdillah Kitota., MMDSC.





وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا 

Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu (Surat Maryam, 19:25).


فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا 


Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu (Surat Maryam, 19:26).


Hapo kinasimuliwa kisa cha Maryam bint ‘Imran wakati wa leba na kujifungua mtoto wake Nabii ‘Isa bin Maryam [Yesu] ‘Alayhis salaam. 


Kwa mujibu wa Tafsir Al-Qur’an Al-‘Adwim ya Al-Imam Ibn Kathir, aliambiwa alishike tawi la mti wa mtende na alitikise. Kwa hiyo, Mola wake Mlezi; ambaye ndiye Mola Mlezi wa Nabii ‘Isa [Yesu] akambariki kwa tende mbichi zilizowiva na maji.


Kimaumbile, swali la msingi tunalopaswa kujiuliza hapa ni kwamba, kwa nini Mola wetu Mlezi (Subhaanahu wata’alah) amwongoze mpaka kwenye mti wa mtende na ambariki kwa tende wakati huu wa leba? 


Kwa tafakuri hii, bila shaka ni lazima kutakuwa na mafungamano ya kimaumbile ya moja kwa moja baina ya ulaji wa tende na leba. Kwa maana kwamba, ulaji wa tende wakati wa leba unafaida za kimaumbile katika kufanikisha leba na kujifungua.


Hii ndiyo ishara ambayo Mola wetu Mlezi (Subhaanahu wata’alah) amewaonesha wataalamu wa tiba hivi karibuni kama alivyoahidi kupitia Qur’an, Surat Fussilat, 41:53. Hapa nitaainisha baadhi ya utafiti.


Hitimisho la makala iliyoandikwa na Rebecca Dokker na kuchapishwa katika mtandao wa https://evidencebasedbirth.com/evidence-eating-dates-to-start-labor/#:~:text=In%20summary%2C%20randomized%20trials%20have,effect%20on%20postpartum%20blood%20loss mnamo Juni 21, 2017 linaeleza:


Uchunguzi unaowajumuisha washiriki [wachunguzwa] kupitia sampuli nasibu (randomised trial) umeonesha kwamba, ulaji wa tende; takribani gramu 60-80 kwa siku, katika wiki za mwisho-mwisho za ujauzito unaongeza kulainika kwa mlango wa kizazi (cervical ripening), unapunguza mahitaji ya kuchochea kuanza kwa leba kitiba (medical labour induction au augmentation), na kupunguza utokaji wa damu nyingi baada ya kujifungua, lochia.


Uchunguzi wa wajawazito 89 wenye anuani ya Effects of date fruit consumption on labour and vaginal delivery in Tabuk, KSA uliofanywa na Ahmed na wenzake, 2018 na kuchapishwa katika jarida la Journal of Taibah University Medical Sciences unaeleza kuwa:


Kuna uhusiano chanya baina ya ulaji wa tende na afya ya mama katika hatua ya kwanza na ya pili ya leba. 


Vilevile, kuna uhusiano chanya baina ya ulaji wa tende na afya ya mtoto kwenye nukta ya afya ya kiowevu, kasi ya mapigo ya moyo ya mtoto, kuwepo kwa uvimbe kichwani kwenye eneo lililo dhidi ya mlango wa kizazi (caput), mwonekano, wizani wa ateri kadiri damu inavyopita (pulse), kujikunja kwa sura (grimace), shughuli na upumuaji.  


Marejeo yaliyowasilishwa katika uchunguzi huu pia yanaeleza kwamba, ulaji wa tende katika wakati wa leba humzidishia mama uwezo wa kuhimili maumivu, na uwezo wa plasma ya damu kupambana na dutu zinazosababisha madhara kwa seli, free radicals. Pia, tende huchukuwa muda mfupi kumeng’enywa ili kutoa nishati (nguvu). Hivyo, humwongezea mama uwezo wa kusukuma mtoto.


Uchunguzi wa randomised trial wa wajawazito 210 (waliokuwa kwenye wiki ya 37-38 ya ujauzito) wenye anuani ya The Effect of Late-Pregnancy Consumption of date Fruits on Cervical Ripening in Nulliparous Women uliofanywa na Kordi na wenzake, 2014 na kuchapishwa katika jarida la Jounal of Midwifery & Reproductive Health umehitimisha kwamba:


Kutanuka kwa mlango wa kizazi kulikuwa ni kukubwa zaidi kwa wajawazito waliokuwa wanakula gramu 70-75 za tende kila siku mpaka mud awa leba ulipofika, ikilinganishwa na wajawazito ambao hawakuwa wanakula tende mpaka muda wa leba ulipofika. 


Marejeo ya uchunguzi huu vilevile yanaeleza kwamba, ulaji wa tende katika wiki za mwisho-mwisho mwa muhula wa ujauzito na wakati wa leba huongeza nafasi ya kujifungua kwa njia ya asili, spontaneous delivery.


Uchunguzi wa wajawazito 80 wenye anuani ya The Effect of Oral Date Syrup on Severity of Labor Pain in Nulliparous uliofanywa na Naavoni na wenzake, 2018 na kuchapishwa katika jarida la Siraz e-Medical Journal umehitimisha kwamba:


Syrup ya tende ina athari ya kupunguza uchungu wa leba kwa wajawazito waliopatiwa, ikilinganishwa na wajawazito ambao hawakupatiwa.


Uchunguzi wa wajawazito 182 wenye anuani Effects of Dates in Late Pregnancy on the Duration of Labor in Nulliparous Women uliofanywa na Kordi na wenzake, 2017 ulihitimisha kwamba:


Ulaji wa gramu 70-76 za tende katika wiki za mwisho-mwisho za ujauzito (kutokea wiki ya 37) unapunguza urefu wa kipindi cha leba na mahitaji ya homini ya kuchochea leba ya oxytocin. 


Uchunguzi huu umependekeza ulaji wa tende bila contraindication, bila ya madhara yoyote. Mapendekezo kama haya vilevile yametolewa na Kordi na wenzake, 2014.


Hitimisho hili linafanana na lile lililotolewa kwenye uchunguzi wenye anuani The effect of late pregnancy consumption of date fruit on labour and delivery uliofanywa na Al-Kuran na wenzake, 2011. Uchunguzi huu nao umehitimisha:


Ulaji wa tende katika kipindi cha wiki 4 kabla ya muda wa matarajio [ya kujifungua] husaidia kupungua kwa muda wa awamu ya kwanza ya leba. Vilevile hupunguza mahitaji ya kuchochea leba kitiba na hutoa matokeo mazuri ya kujifungua.


Kiujumla, ugunduzi huu unatupeleka kwenye swali lingine kwamba, wale ndugu zetu wanaodai kuwa Nabii Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) ndiye mtunzi wa Qur’an [au wanadamu wengine], wanaweza kukubali kwamba majaribio hayo yaliyopelekea kugundulika kwa yote hayo vilevile yalifanyika karne ya 7 wakati Qur’an inatungwa?


Jibu la swali hilo ni hapana. Hawawezi kuikubali hoja hiyo kwa sababu hakukuwa na vifaa, zana, kemikali na mbinu zozote zile kama tulizonazo sasa za kufanyia uchunguzi huu.


Kama hivyo ndivyo, basi haina budi wakubaliane nasi kwamba, Nabii Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wasallam) alikuwa Mtume wa kweli aliyekuwa anapokea ufunuo [wahyi] kutoka kwa Mola wetu Mlezi (Subhaanahu wata’alah). 


Na kwamba, Qur’an ni maneno halisi ya Mola wetu Mlezi (Subhaanahu wata’alah). 


Ndiyo maana utajionea mwenye kwamba, imebainisha kuwa, Maryam alimzaa Nabii ‘Isa (Alayhis salaam); Yesu, chini ya mti wa mtende na kabla ya kuzaliwa [wakati wa leba] alibarikiwa kula tende.


Na bado; kwa mujibu wa aya ya nyuma ya aya hizo (aya ya 24), chini yake alibarikiwa kijito kidogo cha maji kwa ajili ya kunywa; na huenda kwa ajili ya kujifungulia kama wanavyojifungulia baadhi ya wanawake leo hii, water births.


Kwa upande wa pili, kule kwenye Biblia imehadithiwa kwamba Maryam alijifungulia kwenye boma la ng’ombe. 


Hii inatuonesha kwa uwazi kabisa utofauti uliopo baina ya maneno halisi ya Mola wetu Mlezi (Subhaanahu wata’alah) na hadithi za wanadamu.

Shairi la Corona(Covid-19).

MTUNZI: MAULID BIN SWALEH
SHAIRI: CORONA

Janga limeikumba dunia, hatimae tunatanga
Tuiombee dunia, liondoke hili janga
Corona itaondoka, turudi kwa rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Hakika ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana
Kwetu ndio fundisho, tumkumbuke rabbana
Humfaa ukumbusho, anayerudi kwa rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Allah kaleta janga, kuwafunza waja wake
Kutokana na janga, msaada kutoka kwake
Corona ni fundisho, mponaji ni rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Tufanye istighari, atusamehe mola wetu
Tuondoe zetu jeuri, tumsabihi mola wetu
Tufanye masahihisho, atunusuru rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Corona inatumaliza, mkingaji ni rabbana
Ibadani kujituliza, tukimlilia rabbana
Hakika ni fundisho, muondoshaji rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Barakoa tunajikinga, pia kunawa mikono
Allah ndio kinga, tuinue kwake mikono
Mtume ni fundisho, katuletea rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Ushauri tunapewa, wanatoa madaktari
Unaenea kwa hewa, maneno ya madaktari
Bado ni fundisho, kimbilio ni rabbana
Corona ni ukumbusho, kutoka kwa rabbana

Facebook: Maulid Bin Swaleh

Instagram: Maulid Bin Swaleh

Twitter: Maulid Bin Swaleh

Youtube: Maulid Bin Swaleh

Gmail: maulidbinswaleh@gmail.com

Contact no: 🇹🇿🇹🇿🇹🇿 Tanzania +255 756 716 511



*****************MWISHO*****************

Qur'an tukufu ilivyotuelezea umri wa mama kumnyonyesha mtoto katika karne ya saba(7)

Al-Baqarah 2:233

وَٱلْوَٰلِدَٰتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَٰدَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِۖ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ ٱلرَّضَاعَةَۚ وَعَلَى ٱلْمَوْلُودِ لَهُۥ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِٱلْمَعْرُوفِۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَاۚ لَا تُضَآرَّ وَٰلِدَةٌۢ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُۥ بِوَلَدِهِۦۚ وَعَلَى ٱلْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَاۗ وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُوٓا۟ أَوْلَٰدَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّآ ءَاتَيْتُم بِٱلْمَعْرُوفِۗ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ 

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.

Kufunga siku ya tisa (9) na kumi (10) ni bora zaidi kuliko kufunga siku ya kumi (10) na ya kumi na moja (11)



​صيام التاسع مع العاشر أفضل من صيام الحادي عشر مع العاشر.​

*KUFUNGA (SIKU) YA TISA (9) NA KUMI (10) NI BORA ZAIDI KULIKO KUFUNGA SIKU YA KUMI (10) NA YA KUMI NA MOJA (11).*


للعلامة الإمام عبد العزيز بن عبد الله بن باز- رحمه الله-

*(Fatwa) ya Mwanachuoni Mkubwa 'Abdul-'Aziiz bin 'Abdullah bin Baaz-Allah amrahamu-*


السؤال:

*Suali: 🎤*


ما حكم صيام يوم عاشوراء، وهل الأفضل صيام اليوم الذي قبله أم اليوم الذي بعده أم يصومها جميعا أم يصوم يوم عاشوراء فقط ؟ نرجو توضيح ذلك جزاكم الله خيرا.

*​Ni ipi hukumu ya kufunga 'Aashuraa, na je ni bora zaidi kufunga siku ambayo inayofuata au siku (moja) kabla yake au afunge (siku) zote au afunge 'Aashuraa peke yake?​*


نرجو توضيح ذلك جزاكم الله خيرا.

*Tunataraji ufafanuzi wa hilo Allah awalipe kheri.​*


​ الجواب:​

*Jawabu:  📚*

صيام بوم عاشوراء سنة؛

*Kufunga siku ya kumi ya mwezi wa Muharram (mfungo nne) ni sunnah,*


 لما ثبت في الأحاديث الصحيحة عن رسول الله- صلى  الله عليه وسلم من الدلالة علــے ذلك،

*Kwa sababu ya hadithi sahihi sa mtume- swala na salamu zimfikie-zinazojulisha hilo,*


 وأنه كان يوما تصومه اليهود،

*Na hakika hiyo (siku) ni siku (ambayo) Mayahudi walikuwa wakiifunga,*


لأن الله نجى فيه موسى وقومه وأهلك فرعون وقومه،

*Kwa sababu Allah alimuokoa (ndani ya siku hiyo) Musa na watu wake na alimwangamiza Firauni na watu wake,*


 فصامه نبينا محمد - صلــے الله عليه وسلم شكرا لله، وأمر بصيامه،

*Basi akafunga nabii wetu Muhammad kwa kumshukuru Allah, na akaamrisha ifungwe,*


وشرع لنا أن نصوم يوما قبله أو يوما بعده،

*Na akatuwekea (kuwa) ni sunnah tufunge siku (moja) kabla yake au siku (moja) baada yake,*


 وصوم التاسع مع مع العاشر أفضل،

*Na kufunga (siku) ya tisa na ya kumi ni bora zaidi,*


 وإن صام العاشر مع الحادي عشر كفــے ذلك، لمخالفة اليهود،

*Na kama (mtu) akifunga siku ya kumi na ya kumi na moja hilo linatosha kwa ajili ya kwenda kinyume na Mayahudi,*


 وإن صامهما جميعا مع العاشر فلا بأس؛

*Na kama atazifunga (siku) mbili zote (9+11)  pamoja na siku ya kumi basi (hilo) halina ubaya,*


 لما جاء في بعض الروايات:

*Kwa sababu ya (maneno) yaliyokuja katika baadhi ya riwaya (ambayo) ni:*


 ”صوموا  يوما قبله ويوما بعده“

*“Fungeni siku (moja) kabla yake na siku (moja) baada yake”*


 أما صومه وحده فيكره والله ولي التوفبق.

*Ama kuifunga ('Aashuraa) peke yake inachukiza, na Allah ndiye msimamizi wa taufiq.​*


📚 المصدر: ​مجموع فتاوى ابن باز (404/15)

*[ Chanzo: Maj'mu'u fataawa ibn Baaz (15/404​) ]*

*Mfasiri: Abuu Thurayyaa Ismail seiph Mbonde - Allah amuhifadhi*
Dar es salaam, Tanzania 🇹🇿


Watu wa aina saba watakaokuwa katika kivuli cha ALLAH

Watu Aina Saba Watakaokuwa Katika Kivuli Cha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Siku Ya Qiyaamah


Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kuna watu saba (7) ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) atawafunika katika kivuli chake katika siku ambayo kutakuwa hakuna kivuli isipokuwa kivuli chake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)”:

1. Kiongozi Muadilifu;
2. Kijana aliyekulia katika kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa);
3. Muislamu ambaye moyo wake umesehelea katika msikiti;
4. Watu wawili wapendanao kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Kukutana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuachana kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa);
5. Mwanaume aliyeitwa na mwanamke mrembo kwa kutaka kufanya matendo ya haramu na akasema, “La hakika mimi namuogopa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa)”.
6. Mtu anayetoa sadaka kwa mkono wa kulia na wa kushoto usijue kitu kilichotendeka (atoae sadaka kwa siri bila ya wengine kujua kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na
7. Mtu anayemkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa faragha na huku macho yake yakatokwa na machozi.”
[Al-Bukhaariy na Muslim]

Shariy’ah Ya Dini ImekamilikaImaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah)

Shariy’ah Ya Dini Imekamilika

Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah)



Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

Shariy’ah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni shariy’ah iliyokamilika kabisa, haikuacha jambo lolote jema lililojulikana na werevu isipokuwa ameliamrisha. Na hakuacha jambo lolote lillilokua ovu na ambalo limejulikana na werevu isipokua amelikataza. Hakuamrisha jambo na watu wakasema "Laiti kama asingeliamrisha". Na Hakukataza jambo wata wakasema "Laiti kama asingelikataza"

[Al-Bidaayah Wan-Nihaayah (6/79)]

Maulid Bin Swaleh

JINSI ULAJI WA TENDE UNAVYOSAIDIA LEBA YA UZAZI

JINSI ULAJI WA TENDE UNAVYOSAIDIA LEBA YA UZAZI ✍️Abdillah Kitota., MMDSC. وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا...